BINTI WA AJABU AIBUKA, AKILIA ANATOA MAWE BADALA YA MACHOZI

Binti mmoja wa miaka 12, amewaacha madaktari wakikosa jina la ugonjwa unaomsumbua wala tiba, kutokana na kutokwa na mawe badala ya machozi anapolia.
 
Saadiya Saleh, anayeishi nchini Yemen, anatokwa na mawe madogo magumu chini ya kope za macho yake anapolia. Kama ilivyo kwa machozi, mawe hayo huanza kutokeza mbele ya macho, kabla ya kuanguka chini ya mashavu yake.

Video ya binti huyo akilia huku mawe hayo yakimtoka ilionyeshwa na kusambazwa kwenye mitandao na televisheni ya Azal iliyopo nchini Yemen.

Video hiyo inaonyesha Saadiya akiwa amelala kitandani, akiwa amezungukwa na madaktari na jamaa zake, huku akitokwa mawe hayo yaliyokuwa yakidondokea kwenye nguo zake, kama ishara ya machozi. Baadaye daktari alionekana ameshika kusanduku kidogo, kilichojaa mawe yaliyomtoka msichana huyo baada ya kulia kwa saa chache.

Kwa mujibu wa Gazeti la Daily Mirror, madaktari wamesema kuwa hawawezi kuitolea maelezo hali ya Saadiya kwa sababu hadi sasa hawajui ugonjwa unaomsumbua. Hata hivyo, wananchi wamesema hofu yao ni kuwa msichana huyo ameingiliwa na majini au ni mchawi.

“Hali hii imesababisha hofu katika eneo ambalo msichana huyu anaishi,” alisikika mtangazaji alipotoa maelezo katika video hiyo.

“Wengine wanasema msichana huyu anaweza kuwa anatumiwa kwa mambo ya uchawi, huku wengine wakisema inaweza kuwa mashetani. Wengine wanahofia inaweza kuwa mwanzo wa janga la hatari,”alieleza mtangazaji huyo

Imeandaliwa na Herieth Makwetta na Mtandao
Categories:

0 comments: