TUKIO LA AJABU JIJINI DAR: MTOTO AISHI MAKABURINI..!!!
Stori: Haruni Sanchawa na Makongoro Oging’
WAKATI sehemu ya makaburi imekuwa ikiogopwa na watu wengi kutokana na ukweli kwamba ni makazi ya wafu, hali ni tofauti kwa mtoto wa kiume anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 8-9 ambaye jina lake halikuweza kufahamika, kuishi katika makaburi ya Kigilagila, Yombo jijini Dar es Salaam kwa zaidi ya mwezi mmoja.
Taarifa zilizopatikana kutoka eneo la tukio na baadaye kufuatiliwa kwa karibu na waandishi wetu, zinasema mtoto huyo ambaye hafahamiki alikotokea, alionekana akishinda na kulala katika makaburi hayo kwa zaidi ya mwezi mzima uliopita, kabla ya kutoweka kuelekea sehemu isiyojulikana.
Lakini baada ya siku kadhaa za kutoweka kwake, majirani wanasema walimuona tena mtoto huyo akiendelea na maisha eneo hilo ndipo walitoa taarifa Kituo Kidogo cha Polisi Yombo kuwataarifu juu ya tukio hilo lisilo la kawaida.
Polisi walifika makaburini hapo na kumchukuwa kijana huyo lakini walipomuhoji hakuweza kuongea chochote, hali iliyowafanya askari hao kutojua cha kufanya.
Kutokana na hali hiyo, polisi wa Kigilagila walifanya mawasiliano na Kituo cha Buguruni kwa hatua zaidi, ikiwemo kubaini anakotoka na sababu za kuishi katika mazingira hayo.
Gazeti hili lilifika na kumkuta mtoto huyo akiwa katika Kituo cha Buguruni anakohifadhiwa wakati ndugu au wazazi wakisubiriwa, kabla ya taratibu za kumkabidhi kwa Ustawi wa Jamii kuanza kuchukuliwa.
Aidha, vyanzo vyetu ndani ya kituo hicho vilisema kuna watu walijitokeza wakiwa wanatafuta mtoto wa namna hiyo, lakini baada ya kumuona, walisema hakuwa yeye.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, SACP Marietha Minangi alithibitisha kuwepo kwa mtoto huyo na kwamba taratibu zinafanywa ili kulimaliza tatizo lake.
“Natoa wito kwa wananchi waliopotelewa na kijana mwenye umri huo, kufika katika Kituo cha Polisi Buguruni ili kuweza kumtambua mtoto huyo,” alisema Kamanda Minangi.
0 comments: