FAHAMU HAPA FAIDA ZA KULALA USINGIZI,NA MAMBO MENGINE USIYOYAJUA KUHUSU USINGIZI




WATU FULANI HUDHANI kwamba kulala usingizi ni kupoteza wakati. Wao huwa na shughuli nyingi za kibiashara na kirafiki kila siku, na hulala tu wanapokuwa wachovu sana. Kwa upande mwingine, wengine hutamani sana kupata usingizi mtamu lakini hujigeuza-geuza kitandani hadi asubuhi. 

Kwa nini baadhi ya watu hushindwa kulala, hali wengine wanatamani sana kuwa macho? Je, tuuone usingizi kuwa starehe tu au ni muhimu? Ili kujibu maswali hayo, ni lazima tufahamu mambo yanayotukia tunapolala.

Mambo Yasiyojulikana Kuhusu Usingizi 
Kile kinachomfanya mtu apoteze fahamu na kulala usingizi bado hakijulikani. Hata hivyo, watafiti wamegundua kwamba usingizi ni utaratibu tata unaorudiwa na ubongo baada ya kila saa 24.
Tuendeleapo kuzeeka, mazoea yetu ya kulala hubadilika. Mtoto mchanga hulala kwa vipindi vingi vifupi vyenye jumla ya saa 18 hivi kwa siku. Kulingana na wataalamu wa usingizi, watu fulani wazima wanahitaji kulala kwa muda wa saa tatu tu huku wengine wakihitaji muda wa saa kumi.


Uchunguzi wa hivi karibuni unaonyesha pia kwamba vijana fulani huona ugumu wa kuamka asubuhi kwa sababu ya mabadiliko ya utendaji wa mwili. Yaonekana mwili wa vijana hubadilika wanapobalehe, na ndiyo sababu wao hutaka kulala usiku sana na kuamka wakiwa wamechelewa. Mazoea hayo ni ya kawaida nayo huendelea hadi miaka ya katikati na ya mwisho ya ujanani
Utendaji wa miili yetu huongozwa na kemikali zilizo mwilini na tayari nyingi zinajulikana. Mojawapo ya kemikali zinazodhaniwa zinasababisha usingizi ni homoni inayoitwa melatonin. 

Homoni hiyo hutengenezwa kwenye ubongo, na baadhi ya wanasayansi wanaamini kwamba ndiyo inayopunguza utendaji wa mwili kabla tu ya usingizi. Homoni hiyo inapotengenezwa, joto la mwili na damu inayoenda kwenye ubongo hupungua, na pole kwa pole misuli yetu hulegea. Ni nini kinachotukia mtu anapoanza kulala usingizi?

“Njia Kuu ya Asili Inayoburudisha”
Muda wa saa mbili hivi baada ya kulala usingizi, macho yetu huanza kusogea-sogea haraka. Jambo hilo limewafanya wanasayansi wagawanye usingizi katika vipindi viwili: kipindi cha kusogeza macho haraka na kipindi cha kutosogeza macho. 

Kipindi cha kutosogeza macho kinaweza kugawanywa katika vipindi vingine vinne vya usingizi mzito zaidi. Vipindi hivyo viwili hubadilishana mtu anapolala usingizi mzito.

Mara nyingi, mtu huota ndoto wakati wa kipindi cha kusogeza macho. Pia misuli ya mwili hulegea kabisa, na hivyo mtu huamka akiwa mchangamfu. Isitoshe, watafiti fulani wanaamini kwamba habari mpya huhifadhiwa katika kumbukumbu letu la kudumu katika kipindi hicho cha usingizi.


Wakati wa usingizi mzito (kipindi cha 3 na cha 4 cha kutosogeza macho), shinikizo letu la damu na mpigo wa moyo hupungua zaidi, na hivyo kupumzisha mzunguko wa damu na kumwepusha mtu na ugonjwa wa moyo. Zaidi ya hilo, homoni nyingi za ukuzi hutengenezwa wakati wa kipindi cha kutosogeza macho huku miili ya vijana fulani ikitengeneza homoni za ukuzi mara 50 zaidi wakati wa usiku kuliko mchana.
Inaonekana usingizi huathiri pia hamu yetu ya kula. Wanasayansi wamegundua kwamba kwa kweli usingizi ni “njia kuu ya asili inayoburudisha” kama alivyosema Shakespeare. 

Ubongo wetu huona ukosefu wa usingizi kuwa ukosefu wa chakula. Tunapolala, mwili wetu hutengeneza homoni inayoitwa leptin, inayojulisha mwili wetu kwamba tumeshiba. 

Tunapokuwa macho kwa muda mrefu sana, mwili wetu hutengeneza kiasi kidogo cha leptin, na kutufanya tutamani sana chakula cha wanga. Kwa hiyo, kukosa usingizi kunaweza kutufanya tule chakula kingi cha wanga, na hivyo tunenepe kupita kiasi.

Muhimu kwa Afya 
Isitoshe, usingizi huwezesha mwili wetu kuharibu kemikali ambazo inasemekana zinasababisha kansa na kufanya chembe zizeeke. Katika uchunguzi wa hivi karibuni uliofanywa na Chuo Kikuu cha Chicago, wavulana 11 wenye afya waliruhusiwa kulala kwa muda wa saa nne tu kwa siku sita. 


Baada ya kipindi hicho, chembe zao zilifanya kazi kama chembe za watu wenye umri wa miaka 60, na kiwango cha insulini kwenye damu yao kilikuwa kama kile cha mtu mwenye ugonjwa wa sukari! Kukosa usingizi huathiri pia utengenezaji wa chembe nyeupe za damu na homoni iitwayo cortisol, jambo ambalo humfanya mtu apate maambukizo na magonjwa ya damu kwa urahisi.



Bila shaka, usingizi ni muhimu kwa afya ya mwili na ya akili. Kulingana na mtafiti William Dement, mwanzilishi wa kituo cha kwanza cha kuchunguza usingizi katika Chuo Kikuu cha Stanford Marekani, “inaonekana kiwango cha usingizi ambacho mtu hulala ndilo jambo muhimu zaidi ambalo huamua muda atakaoishi.”

 Deborah Suchecki, mtafiti kwenye kituo cha kuchunguza usingizi huko São Paulo, Brazili, anasema hivi: “Kama watu wangalijua jinsi kutolala usingizi kunavyoathiri mwili, hawangalisema kwamba kulala ni kupoteza wakati au ni uvivu.”.

Lakini je, usingizi hupumzisha mwili nyakati zote? Kwa nini watu wengine hulala usiku kucha na bado huamka wakiwa wachovu? Makala inayofuata itakusaidia kutambua baadhi ya matatizo makubwa yanayoletwa na ukosefu wa usingizi na itaeleza jinsi unavyoweza kupata usingizi wa kutosha.


MATOKEO YA KUKOSA USINGIZI
MATOKEO YA MUDA MFUPI 
▪ Kusinzia
▪ Hisia zinazobadilika- badilika
▪ Kusahau mambo kwa muda mfupi
▪ Kushindwa kupanga mambo na kuyatimiza
▪ Kutokuwa makini
MATOKEO YA MUDA MREFU 
▪ Kunenepa kupita kiasi
▪ Kuzeeka mapema
▪ Uchovu
▪ Hatari kubwa ya kupatwa na maambukizo, ugonjwa wa sukari, magonjwa ya moyo, na matatizo ya tumbo
▪ Kusahau mambo sana


KULALA KIDOGO MCHANA 
Je, umewahi kulemewa na usingizi baada ya chakula cha mchana? Hiyo haimaanishi kwamba hukulala vyakutosha. Ni kawaida kusinzia wakati wa mchana kwa sababu joto la mwili hupungua wakati huo. 

Kwa kuongezea, hivi majuzi wanasayansi wamegundua kwamba kuna protini inayoitwa hypocretin, au orexin,inayotengenezwa na ubongo ambayo hutusaidia kuwa macho. Kuna uhusiano gani kati ya hypocretin na chakula?

Tunapokula, mwili hutengeneza homoni inayoitwa leptin ambayo hutufanya tuhisi tumeshiba. Lakini homoni hiyo huzuia utengenezaji wa hypocretin. 

Yaani, kadirileptin inavyokuwa nyingi kwenye ubongo, ndivyo hypocretin inavyopungua na tunahisi usingizi zaidi. Labda hiyo ndiyo sababu katika nchi fulani watu hulala kidogo baada ya kula chakula cha mchana.

0 comments: