BINTI ALILAZIMIKA KUKEKETWA ILI ASOMESHWE HUKO MKOANI MARA...!!
Mtoto ESTER CHARLES (16)
ambaye anasoma kidato cha tatu katika shule ya Sekondari Rebu iliyoko
wilayani Tarime mkoani Mara, alishindwa kujizuia na kudondosha machozi
katika ukumbi wa kantini ya jeshi la polisi wilayani Tarime baada ya
kueleza masaibu aliyokumbana nayo kwa kufanyiwa ukeketaji na wazazi
wake.
Anapofanyiwa
ukeketaji huaminika kuwa mwanamke kamili aliyeondolewa mkosi na ambaye
anastahili kuolewa. Wakati anafanyiwa ukatili huo, Esta alikuwa
anasoma darasa la saba katika shule ya msingi Rebu, ambapo mara baada
ya kukeketwa, anasema alipata maumivu makali ikiwa ni pamoja na kutokwa
na damu nyingi.
Anasema
alikubali kufanyiwa ukeketaji na wazazi wake baada ya kufaulu mtihani
wa darasa la saba na alikuwa na hamu ya kuendelea na masomo, lakini
akapewa masharti na wazazi wake kuwa ili aendelee na masomo lazima
akeketwe.
“Sikuwa
na jinsi, nilijua ningeenda kukumbana na maumivu makali na kwasababu
nilikuwa napenda shule ilinibidi kukeketwa” anaeleza.
Anasema
aliamshwa saa 11:30 alfajiri akiongozana na mama yake na wanawake
wengine watatu alikwenda kuungana na wasichana wenzake waliokuwa kwenye
orodha ya kufanyiwa ukeketaji na kupelekwa mtoni kuogeshwa!
Tuliogeshwa
na kupewa maneno ya ujasiri ili tusilie wakati wa kukeketwa “ anasema
na kuongeza kuwa Ngariba alilipwa kiasi cha Sh. 10,000/= kwa kila
msichana aliyekeketwa (kwa wakati huo). Esta anasema kuna eneo maalum
lililotengwa kwaajili ya shughuli hiyo na msichana hushikwa mikono yake
kwa nyuma na mama aliyekeketwa.
“Baada ya kufika eneo lile, tulitangaziwa na ngariba kuwa kila mmoja awe na wembe wake, ambao ndiyo alitumia kukeketa” anasema.
Anachokumbuka
siku hiyo ni kujikuta tayari amekwisha keketwa huku akitokwa na damu
nyingi na maumivu makali. Anasema baada ya kukeketwa, wasichana wote
waliwekwa katika uangalizi wa akina mama wasaidizi wakiwemo baadhi ya
ngariba, huku wakiwapatia dawa za kienyeji wale wanaovuja damu
iliisiedelee kuvuja.
“Nilishindwa kula, nilikunywa uji tu, siku ya pili nilipata maumivu makali baada ya kuamshwa asubuhi kwenda kuogeshwa” anaeleza.
Wakisikiliza kwa makini ni washiriki wa Kongamano hilo lililokuwa mahususi kwa ajili ya kuibua changamoto zilizopo katika jamii kuhusu suala la ukeketaji |
Anaiomba
serikali, asasi za kiraia na waandishi wa habari kutoa elimu ya
madhara ya ukeketaji kwa watoto wa kike, na kwa ngariba wapewe elimu ya
kutosha dhidi ya madhara ya ukeketaji.
“Wengi
huku Tarime wanafanya hivyo, wakijivunia kukeketwa kutekeleza mila
lakini pia ngariba bado hawajapata elimu ya madhara ya ukeketaji,
naiomba serikalia na wadau wengine watoe elimu zaidi juu ya madhara ya
ukeketaji” anasema na kuongeza kuwa jamii yao huamini kuwa wakimkeketa
motto wa kike huleta Baraka katika familia.
Anasema
baada ya kukeketwa aliumia sana na aliathirika kisaikolojia ikiwemo
kuzomewa nna wasichana wa rika yake ambao hawakuwa tayari kukeketwa.
“Siku
niliyokeketwa, nilipata shida sana, nilikuwa na hofu hata wenzangu
walikuwa wakinicheka, hata nilipopona nilichukua muda kurudi shule,
niliathirika sana” anasema madhara mengine aliyo yapata ni pamoja na
kuchanika sehemu zake za siri, kutokana na kukeketwa akiwa na wasiwasi
kama atajifungua salama siku za baadaye.
“Mimi
nahisi hata wakati wa kujifungua, nitapata matatizo, naomba wazazi
wetu wabadilike waanze kwenda na wakati na watambue kuwa wanapotufanyia
ukeketaji wanatufanyia ukatili wa kijinsia na kilema cha maisha”
anasema.
Anasema
kuwa kuna uwezekano wa wasichana wanaokeketwa kupata virusi vya ukimwi
kutokana na kukeketwa ba ngariba mmoja, ambaye hukeketa zaidi ya
wasichana 50 kwa siku.
Ester
anaahidi kuhakikisha wadogo zake Neema na Happy kuwa hawato keketwa
kwani yeye kashakuwa mkubwa anayejitambua ana kujua kujieleza.
NDOTO ZA BAADAYE ZA ESTA.
“Nitasomea
uandishi wa habari, nitafanya kazi kwa bidii na natamani niwe kama
Waziri wa Maendeleo ya Wanawake, Jinsia na Watoto, Sophia Simba.
Nampenda jinsi anavyo wahudumia wanawake” anasema.
Ameiomba
serikali kupitia jeshi la polisi kuwakamata mangariba wote wanao
husika kufanikisha ukeketaji na kuwafikisha mahakamani, ili sheria
ichukuemkondo wake .
Anaitaka
jamii ya Wakurya kuendeleza watoto wa kike kitaaluma zaidi badala ya
kuwaoza wakiwa katika umri mdogo, na hivyo kushindwa kuhilili kutunza
familia.
Kaimu
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Tarime – Rorya, Emmanuel Mkoma
anasema kuwa jeshi la polisi kwa kushirikiana na wadau wengine wilayani
Tarime, limeanza kutoa mafunzo ya tohara mbadala itakayo iwezesha jamii
kutambua athari za ukeketaji kwa watoto wa kike.
Hisia za mmoja kati ya wanafunzi wa kiume na uelewa wa suala la ukatili wa kijinsia na ukeketaji wilayani Tarime mkoani Mara. |
Wakisikiliza kwa makini ni wadau wa KIVULINI, Jeshi la Polisi na Wanahabari. |
0 comments: