UKATILI..!! BINTI ABAKWA NA BABA YAKE NA KUAMBUKIZWA UKIMWI
Binti anayedaiwa kubakwa na baba yake, kupewa ujauzito na kuambukizwa Ukimwi. Picha na Florence Focus.
“Amini usiamini hizi ni zama za mwisho mwanangu, mimi hili suala bado
haliniingii akilini kabisa, kwani nilizoea kusikia kama hadithi kuwa
mzazi ana uhusiano wa mapenzi na mwanawe, lakini leo hii yamenikuta ya
kunikuta,” haya ni maneno ya Bhoke Mwita (siyo jina halisi), mama mzazi
wa binti anayedaiwa kubakwa na baba yake mzazi kwa miaka minne.
Bhoke anasema kibaya zaidi mwanaye amefanyiwa unyama huo na baba
yake mzazi, huku akimwachia doa ambalo haliwezi kufutika milele ambao ni
ugonjwa wa Ukimwi.
Tukio hilo linamsababisha Bhoke kunyamaza kwanza kabla ya
mahojiano, baadaye anadai binti yake kapewa ujauzito na maambukizi ya
Ukimwi na baba yake, ingawa alikuwa hajitambua kuwa ni mgonjwa hatua
ambayo imemuumiza na kumtia aibu kwenye jamii.
Mkazi huyo wa Mtaa wa Kigera Kibini, Kata ya Kigera, Manispaa ya
Musoma mkoani Mara, anasimlia historia ya maisha yake hadi kuzaa mtoto
huyo wa mwisho nje ya ndoa baada ya mumewe kufariki, lakini hatima
imekuwa kugeuzwa mke mwenza.
Mwita anasita kuendelea na simlizi kabla binti yake aliyefanyiwa
unyama na baba yake, hajasimulia masaibu yake: “Matatizo niliyonayo ni
mengi, Mungu pekee ndiye anayefahamu, bado naongezewa msalaba mzito kama
huu.”
Ghafla anapaza sauti anaita jina la binti yake aliyefanyiwa ukatili,
aliyekuwa chumba kingine na kumtaka aeleze yote yaliyomsibu ili
ulimwengu utambue.
Simulizi za binti
Anatokea binti mrembo ila sura yake inaonyesha unyonge, mrefu,
mwembamba anasalimia kwa sauti ya upole huku akielekea kwenye kiti
kuketi, afya yake siyo ya kuridhisha.
Bila kupoteza muda, binti huyo anadai alianza kuishi na baba yake
mwaka 2002 akiwa anaingia darasa la tatu, baada ya mama yake kupata
kibarua kwenye nyumba ya watawa.
Anasema baba yake alikuwa akiishi na kaka zake wawili wakubwa ambao
walikuwa wamemaliza shule na wakati huo walikuwa wakijihusisha na kazi
za vibarua.
Anasimulia kuwa alipofika darasa la tano, baba yake alikuwa akimfuata
chumbani kabla ya kaka zake hawajarudi nyumbani na kumtaka afanye naye
ngono. Binti huyo anasema kwamba wakati huo alikuwa hafahamu chochote
kuhusu mapenzi.
“Nilipoona baba ananipiga kila siku, nilikubali, akawa anakuja
chumbani kwangu na wakati mwingine ananiita kwake, tukishamaliza
ananiambia niende kwangu kulala, hivyo nikaona kama jambo la kawaida,”
anasimulia binti huyo.
Anaendelea kusema kuwa baada ya kumaliza shule ya msingi mwaka 2009,
alibaki na jukumu la kumhudumia baba yake kama mume wake, jambo ambalo
anadai lilikuwa likimuumiza, hivyo akaamua kuwa wazi ili apate msaada.
“Mwaka 2010 nilikuwa tu nyumbani, kazi yangu ilikuwa kumhudumia baba, kupika na kuchota maji, marafiki zangu hawakuruhusiwa kufika nyumbani, pia sikutakiwa kutoka, nikizungumza na jirani baba anakuwa mkali kama mbogo, nikaamua kumshirikisha dada yangu (anamtaja) ili anisaidie, japo alikuwa akiniuliza kuhusu jambo hilo namkatalia,” anadai.
Baada ya kumweleza dada yake, alimpa mbinu za kutoroka ili amsaidie
kumfikisha kwa mama yao aliyekuwa amehamia Kijiji cha Kabasa, Wilaya ya
Bunda.
Mama mzazi anena
Bhoke anasema baada ya mumewe wa ndoa kufariki mwaka 1989, alianza
uhusiano na mwanamume huyo (anamtaja) alipata mimba na kujifungua binti
huyo Septemba 3, 1994.
“Nilipojifungua mwanamume huyo alinitunza vizuri, alimpenda mwanawe
hivyo sikuhangaika kumlea ingawa alikuwa mume wa mtu, kwa sababu alikuwa
na familia yake,” anasimlia Bhoke.
Anasema kuwa mwaka 2003 alipata kibarua cha upishi nyumba ya watawa
wa Shirika la Utawa mjini hapa, huku akitakiwa kuishi kwenye nyumba hiyo
hivyo ilimlazimu kumtafutia mtoto wake sehemu ya kuishi kutokana na
nyumbani kwake kutokuwapo mtu.
Mama huyo anadai baada ya mwanamume kupata taarifa kuwa mtoto
amepelekwa kuishi kwa babu yake, alimfuata na kumwomba ampe mwanaee
akamlee.
“Sikuwa na sababu za kumnyima mtoto, kwani ni wake, hivyo
nilimkabidhi. Hata hivyo, nyumbani kwake hapakuwa mbali na nilipokuwa
naishi,” anasema Bhoke na kuongeza:
“Kipindi anamchukua alikuwa anaingia darasa la tatu, hivyo alikuwa na
akili ya kutambua zuri na baya, niliamini kama ataona anateseka atarudi
hapa kwa dada zake.”
Anasema yeye aliendelea kufanya kazi nyumba ya watawa kwa miaka
miwili, kisha akarejea nyumbani na kuamua kwenda kijijini kulima.
Bhoke anadai kabla hajaenda kijijini alikuwa akisikia maneno kwa
majirani kuwa, mzazi mwenzike ana uhusiano wa kimapenzi na binti yake,
lakini hakuamini, huku akimtaka binti yake mmoja kufuatilia ukweli wa
tetesi hizo.
Anadai mwaka 2007, binti yake alianza kutaja maovu ya baba yake kwa
dada yake, lakini akimtaka asimweleze mama yake, ingawa alimwambia licha
ya kusema kuwa baba yake akimtaka kimapenzi, hakutamka iwapo
wanajamiiana.
“Baada ya kupata taarifa hizo nilianza kuhisi kitu ila sikuwa na la
kufanya, kwa sababu mtoto mwenyewe hana ushirikiano wa kutosha,” anadai
Bhoke.
Mwaka 2007, binti alimaliza elimu yake ya msingi Shule ya Kamnyonge lakini alishindwa kuendelea na sekondari.
Anadai baada kushindwa, baba yake alimpeleka Shule ya Msingi Nyasho
kurudia darasa la sita, hivyo alimaliza tena darasa la saba mwaka 2009
lakini hakufaulu.
Taarifa zilivyojulikana
Dada yake binti huyo anadai baada ya mdogo wake kukiri baba yake
anajamiiana naye kwa lazima, alimhurumia na kumsihi atoroke na kwamba
atampa nauli aende kwa mama yake kijijini. Anasema alipofika kwa mama
yake alitafutiwa shule akarudia darasa la saba Shule ya Msingi
Kung’ombe, Wilaya ya Bunda mwaka 2011, alifaulu na kujiunga na Sekondari
ya Wariku mwaka 2012.
Anadai baada ya kufunga shule Juni akiwa kidato cha pili,
alimlazimisha mama yake ampe nauli ili aende Musoma kumsalimia baba
yake. Anadai alipofika kwa baba yake hakurejea tena Bunda, zaidi ya baba
yake kumpigia simu mama yake kuwa mtoto wake anateseka hivyo
anamchukulia uhamisho asomee Musoma Mjini.
Anadai mdogo wake alihamia Sekondari ya Nyasho mjini hapa, ambako
alisoma miezi miwili na kuachishwa na baba yake na kumpeleka Kijiji cha
Sirorisimba, wilayani Serengeti kufanya kazi za hotelini.
Hata hivyo, anadai siri ilifichuka baadaye kwamba mdogo wake
alitoroshwa kutokana na ujauzito, hivyo baada ya mimba kukua alishindwa
kuendelea na kazi ili apate nauli ya kurejea kwa mama yake Bunda.
Baada ya kufika kwa mama yake, alimpeleka kupima ingawa binti huyo
alikataa kuwa siyo mjamzito lakini vipimo vilionyesha ana ujauzito.
Mama yake alimpa nauli ya kurudi kwa baba yake kwa sababu alimchukua
kwa madai ya kumsomesha, hivyo hakuona umuhimu wa kumpokea akiwa na hali
hiyo.
Dada yake anaendelea kusema, siku moja alikwenda kumsalimia mdogo
wake na kumkuta akiwa na hali mbaya, hatua iliyomshtua na kumpigia simu
mama yao na ndugu zake wengine ili kumpa msaada wa kumpeleka hospitali.
“Nilimkuta mdogo wangu akiwa na hali ambayo siyo nzuri kwa kweli,
alikuwa kavimba mwili mzima, halafu amejisaidia haja kubwa na ndogo
hapohapo kitandani hakuna msaada, niliumia sana!”
Baada ya kumpeleka hospitali vipimo vilionyesha ana maambukizi ya
virusi vya Ukimwi, walimpa ushauri nasaha na kumwanzishia dawa za kuzuia
maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto.
Anasema binti alikaa nyumbani wiki moja tu na kujifungua mtoto akiwa
amekufa, kufuatia hali hiyo taarifa zililifikia Dawati la Jinsia la
Polisi na kumtia mbaroni mtuhumiwa.
Msaada wa kisheria
Awali, binti huyo alikuwa akipewa msaada na Shirika lisilo la
Serikali la Watoto Wapinge Ukimwi (WWU) mjini hapa kama mtoto anayeishi
katika mazingira magumu, walimsaidia akiwa darasa la kwanza hadi la
saba, baada kuhitimu elimu ya msingi hawakuendelea naye.
Mkurugenzi wa shirika hilo, Sista Marion Haqhes anasema hawezi
kumzungumzia mtoto huyo kwa sababu shirika lake na sheria ya mtoto
haimruhusu ingawa tukio hilo ni kweli.
Polisi wanena
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Paul Kasabago anathibitisha
kuwapo taarifa za ubakaji na kwamba, mtuhumiwa amekuwa akimbaka binti
yake muda mrefu.
Kasabango anasema licha ya mtuhumiwa kumbaka binti yake mara kwa
mara, amemsababishia ujauzito aliojifungua mtoto aliyekufa na vipimo
vimeonyesha amemwambukiza Ukimwi.
Anasema kwa sasa mtuhumiwa yupo rumande kwa mahojiano zaidi na kwamba, atafikishwa mahakamani muda wowote.

0 comments: