TATIZO LA WANAFUNZI 1280 KUKAA CHINI LIMEPATIWA UFUMBUZI NA MBUNGE WAO.
Ukosefu wa madawati katika Shule ya Msingi Kilima A iliyoko
Halmashauri ya Mji wa Kahama mkoani Shinyanga, huenda ukamalizika kufuatia
Mbunge wa Jimbo la Kahama James Lembeli kuahidi kufuatilia magogo yaliyokamatwa
na maliasili ili yatumike kutengenezea madawati.
Lembeli ameyasema leo alipokuwa
mgeni rasmi kwenye Mahafali ya Darasa la saba ya shule hiyo, kufuatia Risala ya
wanafunzi iliyosomwa kwake ikibainisha tatizo kubwa linalowakabili wanafunzi wa
shule hiyo wapatao 1280, kuwa ni ukosefu wa madawati.
Katika Risala hiyo, wanafunzi hao wamemwambia Lembeli
kwamba pamoja na idadi yao kubwa, shule
ina madawati sitini yanayofanya kazi, ambapo kwa kawaida hukaliwa na wanafunzi
Mia moja themanini huku wengine zaidi ya Elfu moja wakikaa chini.
Awali akitoa salam kwenye mahafali
hayo, Diwani wa Kata hiyo Amosi Sipemba ameitaka serikali kuona umuhimu wa
kutumia magogo ya miti yanayokamatwa na Idara ya Maliasili yatumike
kutengenezea madawati katika shule hiyo.
Kufuatia ushauri huo, Lembeli
ameahidi kutumia juhudi zake zote kuwasiliana na idara ya maliasili ili magogo
hayo yatumike kutengeneza madawati hayo huku akiahidi kugharamia matengenezo
yake yote.
Lembeli pia ameahidi kuchangia bati
60 kwa ajili ya kuongeza vyumba vya madarasa katika Shule hiyo, kitu ambacho
amekuwa akikifanya jimboni mwake, ili kuwahamasisha wananchi kuchangia nguvu
zao katika shughuli za maendeleo.
0 comments: