MASKINI BINTI AUGUA KIFAFA AJENGEWA KIBANDA CHA KUKU,ALALA HUMO MCHANA NA USIKU

Binti
wa miaka 20 aliyetambulika Riziki Haji mkazi wa Kijiji cha Kondo mkoa
wa Pwani, wilayani Bagamoyo, yupo kwenye mateso makali kutokana na
ugonjwa wa kifafa unaomsumbua kwa muda mrefu!
Riziki
ambaye aliugua ugonjwa wa kifafa akiwa na umri wa miezi nane, amekuwa
akiishi katika mazingira magumu kiasi cha kufungiwa ndani usiku na
mchana.
Mtangazaji
wa kipindi cha Hatua Tatu ‘Habari Ndio Hii’ cha 100.5 Times FM, Edson
Mkisi Jr, alifika kijijini hapo na kushudia jinsi binti huyo anavyoishi
katika mazingira ya ‘kinyama na mateso’!.
Mkisi
Jr alishuhudia sehemu anayolala binti huyo ikiwa katika mazingira
hatarishi kiasi kwamba yupo hatarini kung’atwa na wadudu wenye sumu kali
kama nyoka, ng’e ama tangu.
Aidha,
imeelezwa kipindi cha mvua na baridi binti huyo huwa katika hali mbaya
zaidi kutokana na makuti yaliyotumika kutengenezewa kibanda hayahimili
hali hizo.
Akisimulia
tukio hilo, jirani wa karibu na sehemu anayoishi Riziki kwa sharti na
kutoandika jina lake, alisema Riziki amekuwa katika maisha mabaya kwa
muda mrefu huku wazazi wake baba na mama wakitupiana mpira mtu sahihi wa
kuishi nae.
“Baba
wa Riziki yupo Zanzibar na anafahamu vizuri sana hali ya mtoto wake
lakini wala hakuna msaada anaotuma….kuna muda mama yake aliamua
kumpelekea lakini siku chache baadae alimrejesha kwa mama yake! Lakini
pamoja na kumrudisha mama pia alimkataa na wasamaria wema wakamchukua na
kuishi nae,” anasema jirani huyo.
Jirani
huyo alibainisha kuwa akiwa anaendelea na maisha kwa msamaria huyo huku
akionekana mwenye afya njema, alikuja bibi yake (mama mzazi wa mama wa
Riziki) na kumchukuwa na kwenda kuishi nae Bagamoyo ambapo siku chache
baadae alimrudisha kwa mama yake mzazi akidai ameshindwa kuishi nae.
Akizungumza
na Mkisi Jr, mama mzazi wa Rikizi, Bi. Asma Ramadhani, alisema mtoto
wake huyo awali alikuwa na afya njema lakini hajua alipatwa na tatizo
gani alipompeleka kwa baba yake Zanzibar.
Kuhusu
kumfungia mtoto wake ndani saa 24, alisema analazimika kufanya hivyo
kutokana na hali yake huku akijitetea kwa kumuachia huru husababisha
matatizo zaidi hasa anapoanguka sehemu yenye mawe.
“Zamani nilikuwa namruhusu anakwenda hata kisimani lakini sasa simruhusu tena kutokana na hali yake,” alisema.
Alipoulizwa
kuhusu kibanda anacholala, alisema kutokana na hali ya Riziki
anashindwa kumlaza na watoto wake wadogo hivyo kwa kuhofia kuwalalalia
watoto hao nyakati za usiku pindi kifafa kitakapomjia.
Hata hivyo, alikiri maisha ya mtoto wake anapolala si mazuri na kuahidi kumhamisha haraka iwezekanavyo.
Naye
Juma Amani Pazi, mwenyekiti wa eneo hilo, mbali na kukiri mazingira ya
Riziki kuwa mabaya, pia alisema alikuwa hana taarifa kama katika eneo
lake kuna mlemavu anayeishi katika mazingira hatari kama hayo.
Na Edson Mkisi Jr
0 comments: