Zitto awaomba wakazi wa Kigoma kumuunga Mkono kwenye Vita yake ndani ya CHADEMA...!!
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amewaomba wakazi wa Mkoa
wa Kigoma kumuunga mkono katika mapambano yake ndani ya chama hicho.
Akizungumza Mjini Kasulu katika mkutano wa
hadhara, Zitto alisema atahakikisha anapigania haki yake ndani ya
Chadema kwa kufuata taratibu zote zilizowekwa kwa mujibu wa Katiba ya
Chama hicho ili aweze kurudishiwa nyadhifa zake, hususan nafasi ya Naibu
Katibu Mkuu wa Chadema, Bara aliyovuliwa na Kamati Kuu Novemba 21,
2013.
“Najua nakabiliwa na vita kubwa ndani ya Chadema,
lakini kwangu mimi (Zitto) hii ni changamoto, naamini nitashinda tu.
Lakini lolote litakalotokea ndani ya Chadema hata kama ni kunifukuza,
nitarudi kwenu ndugu ili tuamue kwa pamoja nini tufanye, wapi twende kwa
pamoja kama tulivyo kwani nguvu ya mamba ipo kwenye maji,” alisema
Zitto.
Amesema kwa kipindi kirefu anaonekana kama msaliti
ndani ya chama na anatuhumiwa kutoa siri za Chadema kwa CCM na
Serikali. “Tuhuma hizi hazina ukweli, nalaumiwa na kubambikiwa mambo
kutokana na msimamo wangu ndani na nje ya chama.
“Watu wa Kigoma ambao ndiyo tulipokea mageuzi
kabla ya wengine, tunaitwa wasaliti ndani ya Chadema, lakini waliokuja
baadaye kutoka mikoa mingine hawa ndiyo wanajiona wasafi. Wapo Watu
waliingia Chadema baada ya kukosa fursa za kugombea huko walipokuwa
awali na sasa wanajifanya ndiyo Chadema damu-damu. Sitoki Chadema ng’o,
labda wanifukuze,” alifafanua Zitto.
“Mnakumbuka misukosuko iliyomkuta
Dr Kabourou (Aman) alipokuwa Kiongozi wa Chadema, pia walimwondoa
Kafulila (David) na sasa mimi (Zitto) natafutwa ili niondolewe. Lazima
tuungane pamoja kutetea masilahi yetu watu wa Kigoma,” aliongeza Zitto.
0 comments: