BABA AMUUA MTOTO WAKE MCHANGA KWA KUMPIGA NA CHUPA YA BIA

Baba aliyetajwa jina moja la Shaban (25), mkazi wa Kimara-Suka, Dar anadaiwa kuhusika katika mauaji ya mtoto wake asiye na hatia, Salma Shaban (miezi sita) kwa kumpiga na chupa ya bia kichwani na kusababisha mshipa mkubwa wa damu kukatika kichwani.
 
Mtoto aliyeuwawa na Baba yake, Shaban.
Akilisimulia Risasi Jumamosi mkasa huo wa kuumiza moyo, mama mzazi wa mtoto huyo, Matlida Amon alieleza kuwa tukio hilo lilijiri maeneo hayo hivi karibuni majira ya 5:00 asubuhi.
Mama huyo alimtaja kwa machungu mzazi mwenzake huyo kuhusika na tukio hilo.
 
Mama mzazi wa mtoto huyo, Matlida Amon.
Alisema kuwa mumewe huyo wa ndoa alimuomba aende kumchajia simu barabarani ambapo alimuacha mdogo wake wa kike mwenye umri wa miaka 13 na mtoto akiwa anacheza kitandani.
 
Alisimulia kuwa aliporudi nyumbani alishangaa kumkuta mdogo wake akilia nje ya nyumba yao.
 
Matlida alisema kuwa alipomuuliza mdogo wake kwa nini alikuwa akiangua kilio, akamwambia kwamba shemeji yake alikuwa akimwambia kuwa anataka kufanya naye mapenzi.
Baba wa mtoto Shaban (25), mkazi wa Kimara-Suka.
Alisema mdogo wake alimwambia kuwa alimsukumiza kitandani akitaka kumbaka ndipo akapiga kelele na kufanikiwa kumchomoka na kukimbilia nje.
Mama wa mtoto huyo aliendelea kusimulia kwamba alipoingia ndani alianza kumlaani mumewe huyo kwa kitendo alichotaka kukifanya kwa mdogo wake ambapo aliishia kuomba msamaha lakini alimwambia ni bora amuombe mdogo wake (shemeji) na siyo yeye.
 
Matilda alisema kuwa baada ya kumwambia hivyo, yeye alianza kukusanya nguo za mdogo wake ampe ili aende nyumbani kwao ndipo mumewe huyo alipochukua kisu alichokiweka pembeni ya godoro na kutaka kumchoma nacho yeye.
 
Hata hivyo, Mungu mkubwa kwani Matilda alisema kuwa alifanikiwa kukidaka na kwa vile kilikuwa kibovu mwanaume alibaki na mpini yeye akabaki na kisu bila mpini.
Alisema alikitupa kisu hicho kupitia dirishani ambapo alipogeuka mumewe, alimzibua kibao kikali usoni kisha akachukua chupa ya bia iliyokuwa tupu ndani na kwenda moja kwa moja kwa mtoto aliyekuwa akicheza kitandani na kumpiga nayo kichwani huku akisema: “Bora tukose wote.”
 
Matilda aliendelea kusimulia huku akilia kuwa baada ya kufanya kitendo hicho baba huyo alikimbia huku yeye akimkimbilia mtoto aliyekuwa akitapatapa kitandani.
Dakika chache baadaye mtoto alizimia hivyo baadhi ya majirani walimkimbiza katika Hospitali ya Boch iliyopo Kimara-Suka, Dar ambapo alipatiwa huduma ya kwanza kisha wakampiga X-Ray na kugundua kuna mshipa mkubwa wa fahamu kichwani ulikuwa umekatika.
 
Baada ya hapo alikimbizwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar. Alipofikishwa aliingizwa kwenye chumba cha upasuaji ili kuokoa maisha yake lakini ilishindikana kwani alifariki dunia.
 
Baada ya kupata taarifa hizo, ndugu pamoja na mama wa mtoto huyo walikwenda katika Kituo cha Polisi cha Mbezi Kwayusuf na kuandikisha taarifa kisha wakapatiwa jalada la kesi namba KMR/RB/1017/2014 na KMR /735/2014- MAUAJI ambapo mtuhumiwa anasakwa na polisi ili kufikishwa kwenye mkono wa sheria.
CREDITS: GPL

0 comments: