VURUGU KUBWA ZATOKEA KAMPENI ZA UDIWANI KATA YA NDULI ,KADA WA CCM AJERUHIWA VIBAYA , MBUNGE MSIGWA AKAMATWA NA POLISI




Polisi  Iringa  wakiyaongoza magari ya  CCM na Chadema ambalo  amepanda  mbunge Msigwa kuingia  kituo cha  polisi baada ya  kuibuka  vurugu kubwa leo

Mbunge  wa  jimbo la Iringa mjini Mchungaji Peter Msigwa akiwa  chini ya ulinzi wa  polisi leo 
Polisi  akiliongoza  gari la  mbunge Msigwa   baada ya  kukamatwa leo kwa  vurugu katika uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya  Nduli 
gari la mbunge Msigwa  likiwa  polisi  usiku  huu 
makada  wa ccm  wakimsaidia kijana Salum aliyejeruhiwa  leo 
MBUNGE  wa  jimbo la Iringa mjini mchungaji Peter Msigwa amekamatwa na  polisi kufuatia vurugu   kubwa  zilizoibuka leo   katika  uchaguzi mdogo  wa udiwani kata ya  Nduli jimbo la Iringa mjini baada ya  wafuasi wa chama  cha Demokrasia na maendeleo (Chadema)  kuwashambulia  wafuasi wa CCM .

Tukio  hilo  limetokea  jioni  ya leo  baada ya  wafuasi wa Chadema  kuwashambulia  kwa mawe na nondo  wafuasi wa CCM na kupelekea  kijana mmoja wa UVCCM Salum Kaita   kujeruhiwa vibaya na kukimbizwa katika Hospital ya  Rufaa ya mkoa  wa Iringa .

Wakizungumzia tukio hilo  baadhi ya mashuhuda waliozungumza na mtandao huu wa matukio daima   walidai kuwa   Chadema  walikuwa na mkutano  eneo la Nduli na  vijana  hao wa CCM  walikuwa  mbali na eneo la mkutano  wakiendelea  na shughuli zao kabla ya  kuvamiwa na makada wa Chadema.

Hata  hivyo  wakati  wa  vurugu  hizo  zikitokea  inadaiwa mbunge Msigwa alikuwa akishuhudia  tukio zima na  kutuhumiwa  kuhusika kufanya  njama  za  kuwashambulia vijana  hao.

Naibu  meya wa Manispaa ya  Iringa Gervas Ndaki  amemweleza mwandishi wa habari hizi kuwa ana    sauti ya mbunge Msigwa inayoelezea  jinsi ambavyo mbunge  huyo alivyopanga  kufanyika kwa  vurugu  hizo.

 Huku  mmoja kati ya makada wa Chadema  mjini hapa akidai  kuwa  CCM ndio  ambao   walihusika na vurugu  hizo kutokana na kupita  eneo hilo la mkutano wa Chadema wakati  wao  hawakuwa na ratiba  ya kufanya mkutano  eneo hilo.

Mwandishi wa habari hizi ameshuhudia  askari wa FFU  mkoa  wa Iringa  wakiwaongoza  wafuasi wa Chadema  zaidi ya  20  waliokuwa katika  gari la matangazo pamoja na mbunge Msigwa ambae  alikuwa  chini ya  ulinzi na kufika kituoni hapo kwa gari lake  la  ubunge .

Kamanda wa  polisi mkoa  wa Iringa Ramadhan Mungi  hakuweza  kupatikana  kuelezea  undani wa   tukio hilo na jitihada za  kumtafuta  zinaendelea  japo  hadi sasa  saa moja  hii  usiku  mbunge Msigwa yupo  kituo cha  polisi  akihojiwa 
CHANZO: MATUKIODAIMA.COM

0 comments: