TAARIFA YA AJALI MBAYA ILIYOUA WATU 22 HUKO RUFIJI
Wananchi wakiangalia daladala iliyopata ajali juzi usiku katika eneo la Kijiji cha Mkupuka, wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani. Picha na Amini Yasini |
Siku
moja baada ya ajali kuua watu 12 wilayani Same, ajali nyingine mbili
mbaya zilizohusisha magari matano zimetokea katika eneo moja wilayani
Rufiji na kuua watu 22, akiwamo kondakta wa gari aina ya Toyota Hiace
ambaye kichwa chake kimetenganishwa na kiwiliwili.
Ajali
hizo zilizopishana kwa dakika chache zilitokea juzi saa 1:00 jioni
katika Kitongoji cha Mkupuka, Kata ya Kibiti na zilisababisha vifo
vingi kutokana na watu 14 waliojeruhiwa katika ajali ya kwanza iliyoua
watu saba, kukanyagwa na gari jingine wakati wakisubiri kupandishwa
kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser la Idara ya Maliasili ili
kupelekwa hospitali.
Habari
kutoka Kituo cha Afya cha Ikwiriri zinaeleza kuwa miili ya watu wawili
ilitenganishwa kichwa na kiwiliwili, maiti tano zilikuwa na vichwa
vilivyopasuka na maiti nyingine zilikuwa zimekatikakatika mifupa.
“Hii
ni ajali mbaya kati ya ajali ambazo nimewahi kuziona maishani,”
alisema mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo, Frank Sixmund Mlangira (30)
ambaye amelazwa Hospitali ya Mchukwi na ambaye ni dereva wa gari aina
ya Toyota Land Cruiser la Idara ya Maliasili ambalo liligongwa katika
ajali ya pili wakati likichukua majeruhi kuwapeleka hospitalini.
“Dereva wa Hiace alikatwa kichwa na kikatenganishwa na kiwiliwili.”
Ajali ilivyokuwa
Kwa
mujibu wa mashuhuda, ajali ya kwanza ilitokea wakati gari ya abiria
aina ya Toyota Hiace lilipojaribu kukwepa lori lililokuwa limeegeshwa
pembeni mwa barabara na badala yake kugongana uso kwa uso na lori aina
ya Mitsubishi Fuso lililokuwa likielekea Dar es Salaam.
Katika ajali hiyo ya kwanza watu saba walikufa papo hapo na wengine zaidi ya 20 kujeruhiwa.
Wakati
juhudi zikifanyika kuokoa majeruhi na kutoa miili ya waliofariki, basi
jingine lililokuwa kwenye mwendokasi likitokea Lindi kwenda Dar es
Salaam, liliwakanyaga majeruhi 14 waliokuwa wakisubiri msaada na
baadaye kugonga gari la Idara ya Maliasili lililokuwa likipakia
majeruhi kuwapeleka hospitali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei alisema dereva mmoja anashikiliwa na polisi wilayani hapa kwa mahojiano.
Kamanda Matei alisema kuwa maiti 19 zimehifadhiwa katika Kituo cha Afya cha Ikwiriri na wawili wapo Kituo cha Afya Kibiti.
Mganga
Mkuu wa Hospitali ya Mchukwi, Dk. Zakaria Lukeba alisema walipokea
majeruhi 13 wa ajali hiyo na kuongeza kuwa kati ya majeruhi hao, wawili
walithibitika kuwa walishafariki kabla ya kufika na kufanya idadi ya
waliofariki kufikia 23, idadi ambayo inatofautiana na takwimu za
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani ambazo zinaonyesha waliofariki eneo la
tukio ni 21. Jana mchana majeruhi mmoja alifariki na idadi ya
waliofariki kufikia 22.
Alisema
majeruhi watano wamehamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa
matibabu zaidi na kuongeza kuwa majeruhi sita tu ndio waliobaki
hospitalini hapo wakiendelea na matibabu.
0 comments: