KUHUSU DAKTARI KUSAHAU KITAMBAA KWENYE TUMBO LA MGONJWA HUKO TABORA
Mkazi wa
wilaya ya Urambo mkoani Tabora, Mwamini Adamu ametolewa mfuko wa kizazi
na kukatwa sehemu ya utumbo baada ya mganga wa idara ya upasuaji katika
wilaya hiyo kusahau kitambaa tumboni kwa mwanamama huyo wakati
akijifungua.
Kutokana
na kumsababishia ulemavu huo kwa uzembe, Mwamini ameifikisha
Halmashauri ya wilaya ya Urambo kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Magharibi
akidai fidia ya Sh milioni 500.
Mwamini
ambaye anadai kuwa alipwe kiasi hicho cha fedha kutokana na uzembe wa
uliofanywa na Dk Jacob Kamanda aliyemfanyia upasuaji wakati wa
kujifungua na kumsababishia aondolewe mfuko wa kizazi pamoja na kukatwa utumbo.
Mwamini pamoja na mumewe Idrisa Jafari katika madai yao wametaka
walipwe fedha hizo kutokana na makosa ya uzembe uliofanywa na wataalamu
wa upasuaji kwa kuacha kitambaa tumboni mwa mama huyo.
Akitoa
ushahidi wake mbele ya Jaji Amir Mruma jana, mama huyo alidai kuwa
Januari 6 mwaka 2011 alijifungua kwa upasuaji baada ya hapo hali yake
ilizidi kuwa mbaya huku akitokwa usaha ukeni na sehemu ya tumbo kwenye
mshono.
Huku
akiongozwa na wakili wa kujitegemea Mussa Kwikima, mama huyo aliiambia
mahakama kuwa hali hiyo ilifanya apelekwe hospitali ya mkoa wa Tabora Kitete bila mafanikio ndipo ikamlazimu kwenda Itigi kwa matibabu zaidi.
Katika uchunguzi wa kitaalamu uliofanywa na madaktari bingwa, Haile Sales ambaye ni raia wa Italia pamoja na Anatole Lukonge wa hospitali hiyo ya Itigi, waligundua kuwa kuna kitu tumboni kama uvimbe hivyo wakalazimika kumfanyia upasuaji mwingine.
Baada
ya upasuaji huo walikuta kitambaa cha rangi ya kijani ambacho kilikuwa
kimeozesha mfuko wa uzazi pamoja na utumbo kugandana na kitambaa hicho
ikabidi kitambaa hicho kutolewa na kusababisha kupasuka kwa utumbo ili
kumnusuru maisha yake.
Naye daktari bingwa wa magonjwa ya akinamama na ambaye ni mganga mkuu wa hospitali ya Itigi, Anatory Lukonge katika ushahidi wake ameiambia mahakama hiyo kuwa alimpokea mlalamikaji akiwa anatokwa na usaha ukeni na sehemu iliyoshonwa.
Dk Lukonge amebainisha
kwamba walipomfanyia upasuaji mama huyo, walikuta utumbo umeshikana na
mfuko wa uzazi huku kukiwa na kitambaa kimeng'ang'ania juu yake.
Alisema
wakati walipojaribu kukiondoa kitambaa hicho kibofu cha mkojo
kilipasuka wakalazimika kumuwekea mpira ili uweze kumsaidia kutolea
uchafu.
Kesi hiyo ya madai namba 13/2011 imeahirishwa hadi Agosti tatu mwaka huu itakapoendelea kusikilizwa kwa upande wa utetezi kuleta mashahidi wake

0 comments: