MAAJABU..!! FISI WANASWA NA SHANGA NA ROZARI KIUNONI BAADA YA MSAKO MKALI WA WANANCHI HUKO MWANZA
MSAKO wa Fisi waliovamia makazi ya Vitongoji vitatu vya Kijiji cha
Hungumalwa Kata ya Hungumarwa wilayani Kwimba mkoani Mwanza, umezua
maajabu.
Maajabu hayo yamehusishwa na imani za kishirikina, baada ya fisi
wawili kati ya 12 waliouawa, kukutwa wamevalishwa shanga na Rozali,
kiunoni.
Msako Mkali
Msako huo wasiku tatu ulioanza juzi (Jumapili) unahusisha mamia ya
wananchi wa Kijiji hicho na vitongoji vyake vya Mwanzabalemi, Mwanega na
Mwang’ombe, wanaotumia siraha za jadi na mbwa wapatao 50.
Habari za ndani kutoka Kijijini humo zimesema kwamba, kabla ya
wananchi hao kuingia ‘vitani’ kusaka wanyama hao ambao baadhi wanadaiwa
kumilikiwa na watu wachache wanaojihusisha na vitendo vya ushirikina,
wazee wa Kijiji na Vitongoji hivyo, walifanya mazindiko (kinga) ya
kujikinga na nguvu za washirikina ambazo zinge kwamisha zoezi hilo.
Wazee wanena
Kwa mujibu wa baadhi ya wazee wa kijiji hicho ambao hawakutaka majina
yao yaandikwe, walisema kuwa makamanda wa jadi wanaoongoza msakao huo
pamoja na mbwa wao, wana kinga za kupambana na imani za kishirikina
vinginevyo wasingeweza kuua fisi wenye shanga na Rozali wanaotumiwa
kishirikina.
Diwani wa Kata ya Hungumalwa Shija Malando akizungumza na waandishi
katika Kijiji hicho jana, alisema wananchi walifikia maamzi ya kufanya
msako huo wa siku tatu, baada ya kundi kubwa la Fisi hao wanaokadiliwa
kuwa zaidi ya 80, kuwa tishio kwa watoto na mifugo.
Alisema kuwa, kwa muda wa miaka miwili iliyopita hadi sasa, licha ya
wanyama hao kuharibu hekali moja ya matunda aina ya Tikiti Maji
yaliyokuwa yamelimwa na mwanchi mmoja, wameua ng’ombe 109, Mbuzi 135,
kondoo 127 na Nguruwe 15 katika Vitongoji hivyo.
“Njooni muone maajabu haya.” Alisema Malando na kufafanua “Jana (juzi Jumapili) wananchi walifanikiwa kuua fisi kumi wawili kati yao wakiwa na maajabu. Mmoja aliukuwa na Rozali kiunoni na mwingine akiwa na shanga kiunoni huku uume wake ukiwa umetahiriwa kama binaadam.”
Alisema fisi waliokutwa na vitu hivyo kiunoni, kwa imani za kabila
la Kisukuma, wanadaiwa kumilikiwa na baadhi ya watu wenye imani za
kishirikina na kwamba, waliuawa majira ya saa 8 hadi saa 10 mchana
kwenye eneo la mlima wa Mwanzabalemi.
Alifafanua kuwa, fisi kumi waliuawa (jumapili) siku ya kwanza ya
msako huo na wengine wawili waliuawa jana asubuhi na kwamba maeneo ya
milima ya Mwanangi katika Kijiji cha Buyobo na Kitongoji cha
Mwanzabalemi yanasadikiwa kuwa na fisi wengi zaidi.
“Pamoja na kushambulia
mifugo yetu, ilifika mahali wananchi walikuwa hawawezi kutembea kwa
uhuru nyakati za usiku na baadhi ya watoto wanaosoma mbali kukatisha
masomo kwa kuhofia kuliwa na fisi hao.” Alieleza Mwenyekiti wa Kijiji cha Hungumalwa, Clement Kaswahili.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mwang’ombe Joseph Kisena alisema hadi
kufikia leo (siku ya tatu ya msako huo) watakuwa wameua fisi wengi zaidi
kutokana na ushirikiano mzuri wa Vitongoji hivyo vinavyotumia mbwa 50
na silaha mbalimbali za jadi ikiwemo mikuki, mapanga na marungu.
Kisena alisema, pamoja na maajabu ya fisi kuvaa shanga na Rozali
kiunoni ambayo wamejionea na kuzua imani za ushirikina kwa baadhi ya
wananchi, hawatarudi nyuma, hadi walitokomeze kundi la wanyama hao
ambalo ni tishio kwa wananchi na mifugo yao.

0 comments: