CHANZO CHA UGONJWA WA AJABU KWA WASICHANA KUANGUKA SHULENI CHATAJWA
Ugonjwa
wa kuanguka na kupiga kelele unaowakumba baadhi ya wasichana katika
shule mbalimbali nchini, umetajwa kusababishwa na maambukizi ya hofu
inayosababisha mwili kupata dalili za magonjwa yasiyokuwepo.
Mtaalamu
wa saikolojia na theolojia, Mchungaji John Rowse kutoka taasisi ya
The Uhakika Christian Education Trust Fund kutoka Mbeya, alisema hayo
hivi karibuni baada ya kutembelea shule zinazopata tatizo hilo mara kwa
mara na kuzungumza na wazazi, wanafunzi na walimu wa shule hiyo.
Alisema
kuna mambo kadhaa yanayochangia kujenga hofu hiyo ambayo mwili
hujitayarisha kuambukizwa, ikiwemo vitisho vya maisha kwa wanafunzi
vinavyotokana na mambo mbalimbali kama vile ugomvi na mabadiliko ambapo
miili yao inahangaika kujihami.
Kwa
mujibu wa Mchungaji huyo, upo uwezekano kuwa baadhi ya wanaoanguka, ni
wasichana wanaonyanyaswa nyumbani, wengine wanafundishwa kujidharau na
wengine wanabaguliwa na kufanyiwa unyanyapaa shuleni.
Sababu
nyingine ya kuanguka kwa wasichana shuleni kwa mujibu wa Mchungaji
Rowse, ni hofu wanayopewa wasichana hao na waganga wa kienyeji
wanaotabiri au kupiga ramli, pamoja na wachungaji au wainjilisti
wanaokemea mapepo huku wakiwashika kichwani, begani au kwenye shingo na
kuwatetemesha wasichana hao.
Mchungaji
Rowse alisisitiza kuwa dawa pekee ya kutibu ugonjwa huo, ni utulivu
kwani wanafunzi hao hususani wasichana huambukizana kwa hofu hivyo
matibabu yake ni kupunguza hofu na mawazo.
“Hofu
hiyo kwa wasichana hao husababishwa kwa imani potofu, waganga wa
kienyeji wanaotabiri au kupiga ramli … waganga hawa wanapenda kujenga
hofu ya uchawi, ili baadaye wajidai kwamba ni wao waliondoa laana na
kuleta uponyaji.
“Dawa ya kusaidia kuzuia matukio hayo ni kuwa na mipango ya kupunguza msongo wa mawazo shuleni, hasa miongoni mwa wasichana,” alisema.
Mchungaji
Rowse alipendekeza machifu na waganga wa jadi wasikaribishwe shuleni
kuwaombea wasichana hao kwa kuwa watawaongezea hofu.
Pia
alipendekeza wachungaji au wainjilisti wanaopenda kushika mtu kichwani,
begani au kwenye shingo na kumtetemesha, wasikaribishwe shuleni kwa
kuwa nao pia ni hatari.
“Hata wale wanaokemea mapepo kwa sauti kubwa na wakati wakifanya hivyo hupenda kumwangalia msichana kwa ukali jicho kwa jicho.
”Katika
mazingira hayo, watoto watapata tena hofu na wakianguka tena
watasema ni pepo, lakini sivyo. Afadhali mchungaji wa amani, amwombee
kila mwanafunzi aliyekumbwa na ugonjwa huo kwa sauti ndogo tu na kwa
upole na upendo na kumfariji na utulivu. Asitamke wazi neno lo lote juu
ya mapepo,” alisisitiza.
Alishauri
kuwa kila shule iwe na mwalimu au mshauri wa kike ambaye hatoi adhabu
kwa wasichana, atakayepaswa kujenga urafiki nao na kuwa karibu nao, ili
wamwamini na kumwelezea mateso yao ya maisha, nyumbani na shuleni.
Alisisitiza
kuwa wanafunzi wa kike wapewe nafasi za kukutana katika vikundi,
ili wajadiliane pamoja kuhusu mambo yoyote, pia walimu wajitahidi
kumpa kila msichana nafasi ya kusikilizwa.
Alitoa
mfano wa Shule ya Msingi Inyonga wilayani Mlele katika Mkoa wa Katavi,
ambayo aliitembelea na kuzungumza wazazi, wanafunzi na walimu wa shule
hiyo.
Alisema
baada ya shule hiyo kuanza kutekeleza ushauri huo, Mwalimu Mkuu wa
shule hiyo, Casto Ismail, alimwambia kuwa kasi ya matukio imepungua.
“Mwalimu
Mkuu huyo alinieleza kuwa wamekuwa na mitihani ya darasa ya saba, ambao
kwa kawaida husababisha msongo wa mawazo kwa wanafunzi, lakini hakuna
mwanafunzi wa darasa ya saba hata mmoja aliyeanguka wakati huo…katika
madarasa mengine ni wachache walioanguka.
“Niliwaambia
walimu wawe na uvumulivu. Mambo yatatulia kweli baada ya mabadiliko ya
imani ya wazazi na jamii… lakini watalaamu bado wanashindwa kuelewa kwa
nini hali hiyo inakutwa sana kwa wasichana na wanawake,” alisema Mchungaji Rowse.
Mwandishi
alifika katika Shule ya Msingi Inyonga na kuzungumza na Mwalimu Ismail,
ambaye alieleza kuwa ugonjwa huo ulidumu kwa zaidi ya miezi sita
tangu ulipowakumba wasichana wanaosoma katika shule hiyo Novemba mwaka
jana.
Alifafanua
kwamba kasi ya kuanguka kwa wasichana hao shuleni hapo imepungua
baada ya kuanza kufanyia kazi ushauri wa Mchungaji Rowse, aliyefika
shuleni hapo na kuzungumza na wanafunzi. Pia alitoa semina kwa
wanafunzi, walimu na wazazi.
>>Ziro99

0 comments: