TAARIFA KAMILI KUHUSU SAKATA LA RAIS KUTEKWA KAMA DR ULIMBOKA
Rais
wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya na Tiba cha
Bugando (Cuhas), mkoani Mwanza, Musa Mdede, ambaye inadaiwa kuwa
alitekwa nyara amepatikana akiwa hajitambui na mwenye uchovu mwingi.
Mdede
alirejeshwa kwenye nyumba alikokuwa amepanga akiwa hoi huku akionekana
kuchoka akiwa hatambui alichotendewa wala waliomtendea.
Mdede
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya
Juu Tanzania (Tahliso), alitoweka Juni 18, mwaka huu katika mazingira
ya kutatanisha, muda mfupi wakati akijiandaa kwenda kurudisha fomu za
kuomba kutetea nafasi yake katika uchaguzi wa viongozi wa serikali hiyo.
Waziri
Mkuu wa serikali ya wanafunzi wa Cuhas, Benjamini Thomas, alisema Mdede
alifikishwa kwenye nyumba alikopanga eneo la Nyakato na kukabidhiwa kwa
mama mwenye nyumba juzi saa tano asubuhi na watu waliojitambulisha ni
wasamaria wema.
“Kwa
mujibu wa mama mwenye nyumba, walifika vijana wawili wanaokadiriwa kuwa
na miaka 30, walijitambulisha ni wafanyabiashara na kueleza kuwa
walimuokota kijiji cha Usagara wilaya ya Misugwi na kumuhifadhi nyumbani
kwao eneo la Igoma,” alieleza.
Alisema:
“Walimuuliza mama mwenye nyumba kama anamtambua kijana huyo na
alivyokubali walimuacha na kuahidi kurudi jana saa tano kumuona, lakini
hadi sasa hawajarudi.”
Thomas
alisema mama huyo alimuuliza Mdede ni kina nani angewapatia taarifa za
kupatikana kwake na kutaja kaka yake ambaye ni mfanyakazi wa benki
ambaye alifika saa nane mchana.
Alisema
baada ya kufika aliwajulisha viongozi wa wanafunzi wa Cuhas na
walipokwenda kumuona Mdede alikuwa bado katika hali mbaya.
“Alitutambua,
lakini hakuweza kueleza lolote lililotokea tangu siku aliyochukuliwa,
alichofanyiwa na wala alikokuwa, zaidi alieleza kuwa amechoka sana na
anahitaji muda mwingi wa kupumzika,” alisema Thomas.
Waziri
Mkuu huyo alisema walimpeleka hospitali ya Rufaa Bugando na kufanyiwa
uchunguzi na madaktari kueleza kuwa hana tatizo lolote na kumruhusu
kwenda nyumbani kupumzika.
“Kwa
sasa amepumzika eneo la tofauti na alikokuwa akiishi, hiyo ni kwa ajili
ya usalama wake, pia yupo chini ya uangalizi wa Polisi,” alisema
Thomas.
Thomas
alisema baada ya kupatikana na polisi kujulishwa, walitaka wanafunzi
kumchukua bila kufanyiwa uchunguzi wowote, lakini waligoma na kutaka
hadi atakapofanyiwa uchunguzi wa kina wa daktari.
“Kwa
hali aliyokuwa nayo inaelekea alinywesha dawa siyo ulevi wa kawaida
hadi mtu apoteze fahamu, ndiyo mana tumetaka uchunguzi wa daktari ambao
wamemfanyia uchunguzi wa awali na kuchukua vipimo vingine ambavyo majibu
yake bado,” alisema Thomas.
Alisema
tukio hilo linawapa shaka kubwa kwa kuwa haijulikani waliomkamata,
walikokuwa wamemuweka na hadi kumrudisha eneo alilokuwa akiishi.
“Usalama wa viongozi na wanafunzi uko shakani wakati wote…tunalitaka
Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina kuanzia kupotea kwake
kunahusishwa na nini na taarifa itolewe kwa umma,” alisema Thomas na
kuongeza:
“Tunataka kujua alipoteaje, alikuwa anafanywa nini, amepatikanaje.”
Alisema
baada ya hali yake kutengamaa wataitisha mkutano na waandishi wa habari
kuona kama anaweza kueleza alikokuwa na yaliyomsibu akiwa huko.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola, alithibitisha kupatikana
kwa Mdede na kusema alipatikana kutokana na ushirikiano wa wasamaria
wema na Jeshi la Polisi.
Aliongeza kuwa aliokotwa akiwa katika hali ya ulevi, bila kueleza ni wa aina gani.
“Alipatikana akiwa hajitambui, akiwa kama amelewa, tunaendelea kumuhoji,” alisema.
Hata
hivyo, alipotakiwa kufafanua zaidi alisema yupo kwenye msafara wa
Makamu wa Rais na kwamba taarifa alizotoa zinatosha na hataweza kutoa
taarifa zaidi ya hizo.
Kwa
mujibu wa Thomas, Juni 18, mwaka huu, saa 10 hadi 12 jioni ulikuwa
ndiyo muda wa mwisho kikanuni kurudisha fomu za kuwania nafasi ya
uongozi katika uchaguzi huo.
Uchaguzi huo umepangwa kufanyika Juni 29, mwaka huu, huku Mdede alitarajiwa kupambana na wagombea wengine wawili.
Wakati
wa kurudisha fomu watu wa karibu na mgombea mwenza wa Mdede, Moses
Madenge, walipanga kurudisha fomu pamoja, lakini walimsubiri bila
kutokea.
SIRI NYUMA YA PAZIA
Kwa
mujibu wa taarifa zilizopatikana kutoka chuoni hapo, enzi za uongozi
wake Mdede aliwahi kuwaeleza kuwa alikuwa akipata mashinikizo kutoka
kwa watu ambao hajawataja wakimtaka atoe tamko kuhusiana na mchakato wa
Katiba mpya ya Tanzania.
Kutokana
na tukio la kupotea kwa Mdede katika mazingira ya kutatanisha, juzi
Spika wa Bunge la Wanafunzi wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DT),
Yuda Gurty, alisema wanafunzi wa vyuo vikuu nchini walitarajia kufanya
mgomo nchi nzima, kushinikiza Jeshi la Polisi kueleza alipo Mwenyekiti
huyo.
Ingawa
hadi sasa haijathibitika kuhusiana na chanzo cha tukio hilo, lakini
kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, makundi kadhaa
yamekuwa yakijipanga kivyama kutafuta kuungwa mkono katika vyuo vikuu.
Tahliso
kama taasisi inayowaunganisha wanafunzi wa vyuo vikuu nchini ina
ushawishi mkubwa wa kisiasa na baadhi ya wanasiasa wanaotafuta nafasi
kubwa za kisiasa wamekuwa wakiitumia kufanikisha malengo yao.
MFARAKANO TAHLISO
Akikabidhi
madaraka kwa Musa Mdede mapema mwaka huu aliyekuwa Mwenyekiti wa
Tahliso, Amon Chakushemeire, alituhumu kwamba wapo wanasiasa wanajipanga
kuitumia kwa urais mwaka 2015.
Aliasa jumuiya hiyo iendelee kuendeshwa kitaaluma na si kisiasa.
“Wapo
wanasiasa wanaotarajia kugombea urais mwaka 2015 wanaingilia uongozi wa
Tahliso kwa utashi wao ili iendeshwe kisiasa, hali iliyosababisha
kutaka kuingiza usiasa na kutuletea wagombea wao katika uchaguzi
uliofanyika mwaka jana,” alisema.
Chakushemeire
alisema licha ya jumuiya hiyo kutegemea taasisi za nje katika
kujiendesha, lakini katiba yao hairuhusu kushirikishwa wanasiasa ikiwamo
kusaidiwa na taasisi zinazojiendesha kisiasa.
Alisema
changamoto inayoikabili Tahliso ni wimbi la wanafunzi wa elimu ya juu
kugubikwa na siasa badala ya kuweka malengo katika elimu
itakayowanufaisha kwa maisha yao ya baadaye.
MATUKIO MENGINE YA UTEKAJI
Ukiacha tukio la kutoweka Mdede, yamewahi kutokea matukio kadhaa ya utekeji na utesaji wa baadhi ya viongozi wa taasisi.
Mwenyekiti
wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka, alitekwa usiku wa
Juni 25 mwaka 2012 na watu wasiojulikana waliokuwa na silaha za moto
ambao walimjeruhi vibaya ikiwemo kumng’oa meno na kucha.
Mwenyekiti
wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda, Mei 5, 2013
alivamiwa na watu wasiojulikana wakati akirejea nyumbani kwake, Mbezi
Juu, Jijini Dar es Salaam.
Kibanda
ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006) Limited
ambayo ni wachapishaji wa magazeti ya Rai, Dimba, Mtanzania, Bingwa na
The African, katika tukio hilo, watu hao walimng’oa meno, kumkata
kidole, kumjeruhi kwa kitu kizito kichwani na kumharibu jicho la
kushoto.
Hadi leo hakuna mtuhumiwa yeyote ambaye amekamatwa na polisi kwa ukatili, mateso na hujuma walizotendewa Kibanda na Ulimboka.

0 comments: