AL SHABAAB YAMUUA MBUNGE NA MLINZI WAKE NCHINI SOMALIA
Wapiganaji wa Kiislamu wa Al Shaabab.
WANAMGAMBO wa Al Shabaab wamedai kuwa wamemuua kwa
kumfyatulia risasi mbunge maarufu mjini Mogadishu. Taarifa zinasema,
Ahmed Mohamud Hayd (Mb) aliuawa baada ya kutoka hotelini ambapo katika
tukio hilo, mlinzi wake pia aliuawa huku Katibu wa Bunge akibaki
amejeruhiwa.
Kundi la Al-Shabaab, ambalo lina uhusiano na lile la al-Qaeda,
limeapa kuendelea na mashambulizi zaidi katika kipindi hiki cha mwezi
mtukufu wa Ramadhani. Wanamgambo hao walipoteza ngome yao mjini
Mogadishu na kuchukuliwa na Vikosi vya Umoja wa Afrika mwaka 2011,
lakini wameendelea na mashambulizi ya mabomu na mauaji mjini humo.
Msemaji wa kundi hilo, Abdulaziz Abu Musab alisema kuwa kundi lake
limemuua kama ilivyopangwa na kuwa wataendelea kuwafuatilia wabunge
wengine ikiwa hawataachana na Bunge nchini humo. Al-Shabaab imekua
ikipigania kuunda taifa la kiislamu nchini Somalia.

0 comments: