VITISHO: NCCR WATAKA SERIKALI IMLINDE KAFULILA
Chama cha NCCR-Mageuzi kimeitaka Serikali kumpa ulinzi wa
kutosha mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila kutokana na vitisho
anavyopata baada ya kusimama kidete bungeni akitaka suala la uchotaji
fedha kwenye akaunti ya Escrow kutoka Benki Kuu (BoT) lichunguzwe.
Kafulila aliingia kwenye mgogoro na Mwanasheria
Mkuu Jaji Fredrick Werema mwezi uliopita wakati wa Bunge la Bajeti
alipoibua tena suala la wizi wa fedha hizo. Wawili hao walizozana baada
ya Kafulila kuomba mwongozo ambapo Jaji Werema kudiriki kumuita mbunge
huyo “tumbiri”.
Neno hilo lilimfanya Kafulila amwambie Jaji Werema
kuwa naye “ni mwizi” na ndipo baada ya kikao hicho, kigogo huyo wa
serikali alimfuata nje akionekana kutaka kumpiga kabla hajazuiwa na
wabunge wengine. Siku iliyofuata, Werema alikaririwa akisema “anataka
kichwa chake (Kafulila).
Jana, NCCR-Mageuzi iliamua kuomba hadharani ulinzi
wa mbunge wao na kumtaka Jaji Werema ajipime kutokana na vitendo vyake
kama anastahili kuendelea kushika wadhifa huo.
“Kama chama tunapenda kurejea na kusisitiza kuwa
tuna hofu na uhai wa mbunge wetu (Kafulila) hasa kutokana na mazingira
yanayozunguka ajenda hii anayoisimamia ambayo inagusa vigogo na mafisadi
wakubwa,” alisema katibu mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe
alipozungumza na waandishi wa habari jana akiwa pamoja na Kafulila.
“Tunahofia usalama wa Kafulila kwa kuwa Spika Anne
Makinda kashindwa kuchukulia kwa uzito mwongozo ulioombwa na mbunge
huyo kuhusu kutishiwa maisha.
“Tunao uzoefu wa mazingira kama haya kama pale
kijana Amina Chifupa alipozungumzia dawa za kulevya. Pia tunao uzoefu na
kilichotokea kwa Dk Sengondo Mvungi alipokuwa mhimili imara wa serikali
tatu ndani ya tume ya (Jaji Joseph) Warioba, wote tunafahamu
kilichowakuta.”
Akaunti hiyo ya Tegeta Escrow ilifunguliwa baada
ya kuwepo mgogoro wa kimkataba baina ya Shirika la Umeme Tanzania
(Tanesco) na Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kwa
ajili ya kuhifadhi fedha ambazo zingetumika kulipia gharama na malipo
mengine wakati na baada ya mgogoro huo kumalizika kwa maridhiano ya
pande zote mbili.
Nyambabe, aliyekuwa ameongozana na Kafulila akiwa
na nyaraka lukuki alizobainisha ni ushahidi wa ufisadi wa Escrow na
IPTL, alisema jitihada zao za kupambana na ufisadi hazitakoma licha ya
vitisho wanavyopewa.
“Tunataka Serikali kuchukua hatua madhubuti kuhusu
ufisadi huu.
Haturidhishwi na hatua zinazochukuliwa. Tutafanya
utaratibu wa kuwasiliana na vyama ndani ya Ukawa (Umoja wa Katiba ya
Wananchi) kuona namna bora zaidi ya kulisukuma suala hili ili Watanzania
waelewe namna nchi yao inavyotafunwa,” alisema.
“Kama chama, kwa kuwa Bunge na vyombo vya dola
havioni umuhimu huo, tunamwachia Mungu, lakini chochote kikitokea
tunafahamu ushiriki wa Serikali na vyombo vyake.”
Kwa upande wake Kafulila alisema hatishwi na
mahakama wala wanaotaka ‘kumkata kichwa’ na yupo tayari kufungwa kwa
sababu anachokifanya ni kwa masilahi ya umma.“Mimi naziomba taasisi zote zisizo za kiserikali, viongozi wa dini na
wananchi waone kuwa hili jambo nao linawahusu. Hii ‘assignment’ (kazi)
siyo ya Kafulila pekee. Kama nchi nzima tutaungana, hao watakaokuwa
wanaua, wataua wangapi?” alihoji Kafulila.

0 comments: