NA HUKO MTWARA VIONGOZI WA CHADEMA WASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI
CHAMA
Cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema), Wilaya ya Mtwara Mjini, jana
walishindwa kuandamana baada ya Jeshi la Polisi mkoani hapa,
kuwashikilia viongozi wa chama hicho kuanzia saa moja asubuhi hadi sita
mchana.
Maandamano
hayo yalitarajiwa kufanyika kuanzia maeneo ya Makanaledi kupitia
Mnarani, barabara ya Zambia, Stendi Kuu, Madukani, Bima, Coco Beach hadi
viwanja vya Mashujaa, ambako wangezungumza na wananchi, lakini
yalidhibitiwa na polisi ambao walionekana wakirandaranda kila kona
pamoja na magari ya JWTZ kuhakikisha hakuna maandamano hayo.
Viongozi
walioshikikiwa na polisi ni pamoja na Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya
Mtwara Mjini, Ibrahimu Mandoa, Mkufunzi Chadema Mkoa, Ismail Liuyo,
Katibu Stanslaus Sumi na Katibu Mwenezi Hassani Mbangile.
Akizungumza
na Waandishi wa Habari mara baada ya kutoka kituo cha Polisi Wilaya,
Mwenyekiti huyo wa Wilaya, Ibrahimu Mandoa, alisema jana Chadema Wilaya
walikusudia kufanya maandamano ya amani katika Manispaa ya
Mtwara-Mikindani kupinga kuendelea kwa Bunge maalum la Katiba
linaloendelea Dodoma.
Alisema
kuwa, kimsingi kila mtu atakuwa anaelewa kuwa Rais Kikwete na vyama vya
siasa ambavyo viko chini ya TCD, walikuwabaliana kwa pamoja kwamba
hakuna uwezekano wa kuweza kupatikana Katiba mpya sasa hivi mpaka 2016
ndio zoezi la mchakato mzima liendelee.
Kwa
upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Augustine Ollomi,
alithibitisha kukamatwa kwa viongozi hao na kuhojiwa kwa sababu ya
kusambaza vipeperushi kwa wananchi.
Ollomi,
alisema kuwa viongozi wa Chadema walitoa taarifa ya kufanya mkutano
Septemba 21, lakini Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD), Andrew Ndassa,
aliwakatalia kwa sababu zilizotolewa zilikuwa kinyume, wao walitaka
kufanya mkutano kupinga Bunge maalumu ambalo linaendelea Dodoma, na kwa
ufahamu wake bunge hilo liko kisheria sio kama wanavyodai Chadema.
Alisema,
juzi walipata vipeperushi ambavyo vilikuwa vimeandaliwa na viongozi
Chadema mkoani hapa wakiwashawishi wananchi washiriki katika maandamano,
hivyo ndio sababu ya kuwaita kwa ajili ya mahojiano.

0 comments: