NOAH NYEUSI ZAHISIWA KUTEKA WATOTO DAR,ZAWAVIZIA WAKITOKA SHULE.

Lile sakata la utekaji na upoteaji wa watoto ambao wengi ni wanafunzi wa shule za msingi katika Jiji la Dar na kudaiwa linafanywa na watu walio kwenye magari aina ya Toyota Noah limeingia katika sura nyingine.
Safari hii, gari moja lilitupiwa mawe na dereva nusura kuuawa
kufuatia kufika katika Shule za Msingi za Kombo na Mtakuja zilizopo
Vingunguti, Dar kwa lengo la kuzungumza na walimu kuhusu mikopo lakini
likahofiwa lilikwenda kuteka watoto.
Tukio hilo lilijiri Ijumaa iliyopita na kusababisha vurugu kubwa kati
ya wazazi na walimu hali iliyowafanya maafande wa Kituo cha Polisi
Buguruni kuwasili katika eneo la tukio ili kutuliza ghasia na kwanusuru
walimu.
Uwazi lilifika eneo la
tukio muda mfupi na kuwakuta walimu wakiwa chini ya ulinzi wa polisi
ili wasishambuliwe na wazazi ambao walivamia shule wakidai kwamba watoto
watatu walitekwa na watu wenye Noah jeusi.
Vurugu hizo zilizoanza saa nne
asubuhi siku hiyo zilitokea baada ya gari moja jeusi aina ya Toyota Noah
kufika shuleni hapo na kushambuliwa na wananchi wakidai kwamba ndilo
linalotumika kuwatekea watoto wao shuleni hapo.
Mmoja wa wazazi aliyejitambulisha kwa jina la Huma Selemani alisema
Noah hilo la mikopo kwa walimu lililokuwa na vioo vyeusi lilihisiwa ni
la utekaji baada ya jana yake (Alhamisi) ambapo gari kama hilo lilifika
shuleni hapo na dereva kumuuliza mmoja wa wanafunzi sehemu hiyo inaitwaje ambapo
mwanafunzi huyo alisema haijui.
Ilidaiwa kuwa, pamoja na denti huyo kusema haijui sehemu hiyo
walimchukua na kumuingiza ndani ya gari hilo ili kuondoka naye lakini
mzazi mmoja aliona na kupiga kelele huku akilishambulia kwa mawe gari
hilo hadi walipomshusha mwanafunzi huyo na wao kutimka.
Mayowe hayo
yaliwafanya wazazi kuvamia shule hizo na kusababisha wanafunzi kutoka
madarasani huku wengine wakiruka ukuta na kukimbilia majumbani na baadhi
kwenda kusikojulikana.
Wazazi waliokuwa karibu na shule hizo walifika na kuwachukua watoto
wao kisha kwenda nyumbani huku wengine wakitegemea msaada toka polisi
ambao walipofika walifyatua risasi hewani kuwatawanya wananchi hao.
Hata hivyo, walimu wakuu wa
shule hizo hawakupatikana mara moja lakini mwalimu mmoja ambaye
hakupenda jina lake liandikwe alisema hakuna utekaji wa watoto
shuleni bali baadhi ya watu wamekuwa wakivumisha habari hizo na hivyo
kuwatia hofu watoto.
Baadhi ya watu walioongea na Uwazi walisema kuwa, wana taarifa mbaya kwamba watekaji hao
wakishawapata watoto huenda kuwaua ili kutwaa viungo vyao kwa ajili ya
ushirikina wa kupata utajiri.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa
wa Kombo, Jastin John Chiganga alipohojiwa alikiri kutokea kwa vurugu
hizo hali iliyomfanya awaite polisi kutuliza ghasia lakini alisema kwa
upande wa kutekwa watoto na gari aina ya Noah hajawahi kusikia.
“Shule ilibidi ifungwe, watoto waruhusiwe kutawanyika hadi hapo
taarifa itakapotolewa. Hata hivyo, wazazi wameniomba kwamba kabla watoto
wao hawajarejea shuleni hapo anatakiwa kiongozi wa juu, awe DC (mkuu wa
wilaya) au yeyote afike kutoa tamko na kuweka mambo ili kuwatoa hofu
wazazi na wanafunzi,” alisema mwenyekiti huyo.
Polisi wa Buguruni waliokuwepo kwenye tukio hilo walisema hawana
taarifa ya watu waliojeruhiwa au kukamatwa bali zoezi la kudhibiti
amani lilifanyika kwa uangalifu wa hali ya juu.
Wakati huohuo, wazazi wa mwanafunzi Hadija Hansi (10) anayesoma
darasa la nne Shule ya Msingi Magomeni, Dar wanahaha kumtafuta mtoto wao
huyo ambaye alitoweka katika mazingira ya kutatanisha ikidaiwa alitekwa
na Noah.


0 comments: