TAARIFA YA AJALI YA GARI ILIYOUWA WANA NDUGU 12 MKOANI KILIMANJARO WAKATI WAKIENDA MSIBANI..!!
| Lori la mizigo aina ya Fusso likiwa limegongana na gari ndogo aina ya Toyota Hilux Pick Up katika eneo la Hedaru, wilayani Same, Kilimanjaro, juzi na kusababisha vifo vya watu 12. |
Waombolezaji
hao wanawake, walipewa lifti ya gari na Diwani wa Kata ya Hedaru,
Gerard Mgwena (CCM), kwa ajili ya kuwapeleka msibani eneo la Majengo
ambako mtu mmoja alifariki kwa kusombwa na maji.
Kamanda
wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro (RPC), Robert Boaz alithibitisha ajali
hiyo akisema ilitokea juzi saa 2:00 usiku na kwamba ilikuwa mbaya zaidi
tangu kuanza kwa mwaka 2014.
“Ni
ajali iliyohusisha magari matatu kwa wakati mmoja…; watu 11 walifariki
pale pale na mwingine alifariki dunia leo (jana), asubuhi Hospitali ya
Rufaa ya KCMC,”alisema Boaz.
Hata
hivyo, alisema hakuwa na nafasi nzuri ya kufafanua kwa undani ajali
hiyo kwa vile alikuwa nje ya Mkoa wa Kilimanjaro na kuelekeza atafutwe
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa (RTO), Joseph Mwakabonga.
Akizungumza
kwa niaba ya RPC, Mwakabonga alisema, lori aina ya Mitsubish Fusso
lililokuwa likitokea Moshi kwenda Dar liligonga kwa nyuma gari aina ya
Toyota Hilux Pick-Up.
Alisema
kuwa baada ya kuligonga gari hilo lililowabeba waombolezaji hao, nalo
lilisukumwa na kwenda kuligonga lori aina ya Scania lililokuwa na tela
lake.
Lori
hilo aina ya Scania lilikuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Moshi
likiendeshwa na dereva wake, Gabriel David. Madareva wawili wa Toyota
Pick-Up na Toyota Fusso wote hawajulikani waliko.
Taarifa
zilizopatikana baadaye, zilisema dereva wa Fusso alikuwa amelazwa
katika Hospitali ya KCMC, wakati Kigogo wa CCM aliyekuwa amewabeba
waombolezaji akilazwa hospitali moja jijini Arusha.
Mwakabonga
aliwataja waliofariki kuwa ni Stella John(45), Salma Kizoka (33),
Marry Senzige (49), Neema Daniel (52), Rehema George (29) na Sophia
Mbike (51).
Wengine
ni Ritha Kalani (55), Mama Kalani Stephano (55), Kolina Mmatha(55),
Bahati Daud(25) na Farida Kiondo mwenye umri wa miaka 25.
Majeruhi
mmoja, Maria John (33) ambaye ni miongoni mwa watu 10 waliojeruhiwa,
alifariki dunia jana asubuhi katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC
alikolazwa kwa ajili ya kuokoa maisha yake.
Alex Shirima mmoja wa mashuhuda alisimulia kuwa gari la diwani lilikwama kweye tope katikati ya Barabara ya Moshi Dar es Salaam.
Alisema,
kabla ya kushuka kuangalia namna ya kulinasua gari lake, likatokea
lori gari aina ya Fuso kwa nyuma ambalo liliigonga gari lake iwani na
kulisukuma mita kadhaa mbele ambako lilikutana uso kwa uso na lori
lingine aina ya Scania lililokuwa likitokea Dar es Salaam.
Alisimulia kuwa kutokana na ukubwa wa ajali hiyo, eneo hilo lilitapakaa viungo vya binadamu na damu.
Shirima
ambaye ni dereva aliyefika katika eneo hilo dakika mbili baada ya
ajali kutokea, alisema eneo hilo ni hatari kwa madereva kwa kuwa mvua
zikinyesha, barabara hujaa maji na matope.
Alisema
kuwa ajali hiyo imechukua maisha ya ndugu zake wanane na kati ya hao,
saba walikuwa wakiishi kijijini hapo kwenye nyumba tofauti
zinazofuatana.
Kwa
mujibu wa watu walioshuhudia ajali hiyo, watu hao walipata ajali hatua
10 kutoka katika eneo ambalo ndugu yao aliosombwa na maji na kufa,
ambapo maiti yake iliokotwa eneo hilo.
Hali ilivyo kijijini
Mmoja
wa watoto ambaye mama yake mzazi amefariki katika ajali hiyo, Sebali
Mkwizu alisema kuwa kijiji chao kimekumbwa na ukimya na majonzi, huku
wakishindwa kuamini kilichotokea.
“Nimepoteza
mama yangu mzazi, mama mdogo, shemeji zangu watatu, mke wa ndugu yangu
na watoto wawili. Hapa nyumba saba zina msiba,” alisema Mkwizu.
Alibainisha kwamba mazishi ya wanawake hao yanatarajiwa kufanyika leo katika eneo la pamoja kijijini hapo.
“Tumeambiwa watazikwa eneo moja, lakini bado hatujajua ni sehemu gani, hadi kesho (leo) ndiyo tutapata taarifa kamili,” alisema.
Na Daniel Mjema na Rehema Matowo
0 comments: